Rais Obama Marekani ametofautiana na Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kuhusu kuchapishwa hadharani kwa picha za mwili wa Kiongozi wa Kikundi cha Ugaidi cha Al Qaeda, Osama bin Laden.Wakati Mkurugenzi huyo, Leon Panetta akisema picha hizo zitatolewa hadharani kuzima ubishi unaoendelea iwapo kweli mwasisi na kiongozi huyo wa al-Qaeda ameuawa na makomando wa Marekani nchini Pakistan usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, bosi wake amepingana naye.
Jumapili, Panetta, ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais Obama kuwa Waziri wa Ulinzi, aligeuka shujaa machoni mwa wengi kwa kuisimamia vyema operesheni hiyo.
Kufikia juzi, Obama alimpinga, akisema hakuna haja ya kutoa picha za kutisha za mwili huku akiungwa mkono na mawaziri wake wawili akiwamo Waziri wa Ulinzi anayeondoka, Robert Gates na Waziri wa Mambo ya Nje, Hillary Clinton.
Akitangaza uamuzi huo, Obama alisema: ‘Hatuhitaji kushindana kama mpira wa miguu katika suala hili baada ya usiku wa kujivunia wa shambulio wiki hii.”
Rais Obama amesema picha za mwili wa Osama zina uwezekano mkubwa wa kuchochea chuki iwapo zitatolewa.
Maofisa wa Marekani wamekuwa wakijadili iwapo wachapishe picha hizo kukabiliana na nadharia kwamba nchi hiyo imedanganya.
Lakini Obama anaamini kuwa picha hizo huenda zikazua hisia kali akisema:“sisi hatutaki kuonyesha picha hizi kama kikombe cha kujivunia cha kumwonyesha kila mtu.”
Kutofautiana huko kunaonesha mgawanyiko uliopo miongoni mwa maofisa waandamizi wa utawala huo kuhusu kutoa au kutotoa hadharani picha hizo.
Hilo limekuja chini ya saa 72 baada ya kipindi kizuri cha urais wa Obama.
Tofauti hiyo iko hadi kwa Wamarekani ikiwa haihusiani na siasa kwa sababu baadhi ya wanachama wa Republican na Democrat wameunga mkono uamuzi wa rais wa kutotoa picha hizo wakati wanachama wengine wa vyama hivyo wamemkosoa vikali rais.
Wabunge kadhaa na wasaidizi wa Ikulu walieleza kushangazwa kuona tukio kubwa la kumuua gaidi hatari duniani linavuruga furaha na ushindi uliopatikana.
Kwa sasa utawala wa Rais Obama pia unahangaika kufuta ukungu wa shaka kutokana na mkanganyiko wa taarifa zake juu ya mauaji ya kiongozi huyo wa al-Qaida yaliyotokea Abbottabad, Pakistan.
Ikulu ya Marekani inasema kwamba kilichosababisha taarifa za mwanzo kuhusiana na kifo hicho zisiwe kamili ni kile inachokiita ‘ukungu wa vita’.
Kikiwanukuu maofisa wa Ikulu hiyo, kituo cha televisheni cha NBC kimesema watu wote wanne waliouawa, akiwemo Bin Laden mwenyewe, hawakuwa na silaha.
Taarifa hiyo ni tofauti na mbili za mwanzo, ambazo nazo pia zilitofautiana.
Ya kwanza ilikuwa ya Rais Obama mwenyewe akitangaza kifo cha Bina Laden, ambayo alisema kiongozi huyo wa al-Qaida alikufa kutokana na majibizano ya risasi kati yake na makomando wa Marekani.
Ya pili ilitoka kwa Msemaji wa Ikulu Marekani, Jan Carney ambaye alisema kuwa si Bin Laden aliyekuwa amejihami kwa silaha, bali ni wenzake.
Hata hivyo, picha zilizochapishwa na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) zinaonyesha maiti za wanaume watatu zikiwa kwenye madimbwi ya damu, lakini hakuna silaha inayoonekana karibu yao.
Licha ya hayo, Rais Obama amekataa katakata kuchapisha picha za mkasa mzima ulivyokwenda, akirejea msimamo wa Ikulu yake kuwa zitakuwa kichocheo zaidi wafuasi wa Bin Laden.
“Hakuna shaka kuwa tumemuua Osama bin Laden, Lakini ni muhimu kwetu kuhakikisha picha zinazoonyesha mtu aliyepigwa risasi kichwani, hazisambai na kuwa kichocheo cha vurugu na silaha ya kufanyia propaganda,” Rais Obama alikaririwa akisema juzi.
Mwanasheria Mkuu Marekani, Eric Holder, amesisitiza msimamo wa serikali kwamba kuuawa kwa Bin Laden hakukukiuka sheria yoyote ya kimataifa, kwa vile makomando wa Marekani walishambuliwa kwanza na ndipo nao wakalazimika kujihami.
Mwanzoni, mauaji ya Bin Laden yalianza kuijenga upya taswira ya Rais Obama kwa Wamarekani, ambao waliyapokea kwa vifijo na nderemo wakiamini kuwa kiongozi wao amesimamia kauli yake aliyoitoa tangu mwanzo.
“Nina furaha kwamba tuna rais ambaye amehakikisha jambo hili kalikamilisha. Na siyo rais ambaye amepoteza lengo, kama alivyokuwa George Bush, ambaye badala ya kumshughulikia Osama, akajielekeza Irak. Nafikiri hivi alivyofanya Obama ndivyo serikali makini inavyotakiwa iwe,” anasema Tyler, kijana wa miaka 30 anayeishi mjini Washington.
Matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa kwa ushirikiano wa Reuters na kampuni ya Ipsos na kuchapishwa Jumanne, yalionyesha kuwa mauaji ya Bin Laden yamepandisha imani ya Wamarekani kwa Rais Obama, ambaye anakabiliwa na uchaguzi hapo mwakani, wakiamini ameonyesha uongozi mzuri panapohusika suala la vita dhidi ya ugaidi.
Lakini kuanza kuibuka kwa taarifa mpya kila siku kuhusiana na namna mauaji yenyewe yalivyotokea, huku kila taarifa mpya ikipingana na nyingine na wasaidizi wa Ikulu wakitofautiana kuhusu utoaji picha, kumezua wasiwasi na kubadili maoni ya watu, si ndani ya Marekani tu, bali hata nje.
Wakati huohuo kiongozi mpya wa al-Qaeda ameelezea mpango wa mashambulio Uingereza katika barua pepe aliyomtumia mwandishi mmoja kachero wa gazeti la the Sun.
Anwar al-Awlaki anayeishi Yemen na ambaye anaaminiwa atakuwa badala ya Osama Bin Laden, ametaka mashambulio kama ya Mumbai, India, yafanywe Uingereza.
Majasusi wa Shirika la Ujasusi la Uingereza (M16) jana usiku walikuwa wakichunguza mawasiliano yake kwneye mtandao wa intaneti.
Katika barua yake pepe alisema: Tunachoweza kufanya ni kulipua mabomu katika maeneo mbalimbali, kufanya mauaji au kuyafyatulia risasi makundi ya adui.”
Pendekezo la mwisho linaelekea kuonyesha mashambulio ya mabomi yaliyotokea Mumbai, India ambako watu 164 waliuawa mwaka 2008.
Awlaki (40), amekwisha kuongoza majaribio ya mashambulio Uingereza na Marekani.
Alimshawishi mwanafunzi mwenye umri wa miaka 21, Roshonara Choudhry kumchoma kisu Mbunge wa Chama cha Labour, Stephen Timms kwa kuunga mkono uvamizi wa Marekani na Uingereza nchini Irak.