Zaidi ya wawakilishi elfu mbili wa makundi yaliyoshiriki katika maandamano kumfanya Rais Hosni Mubarak aondoke mwezi Februari, wanakutana leo nchini Misri kwa mara ya kwanza, kupanga mustakbali wa siasa wa nchi hiyo.
Tangu Rais Mubarak kuondoka madarakani, Misri imekuwa ikiongozwa na halmashauri ya siri ya kijeshi; wanaharakati walioanzisha maandamano katika medani ya Tahrir hawakuchangia katika mabadiliko yanayotokea.
Katika mkutano wa mwanzo wa Halmashauri ya Taifa ya demokrasi, wanaharakati wanataraji kuwa wataweza kukubaliana juu ya njia za kuendeleza shime katika mapinduzi.
Wasi wasi wao mkubwa ni kuwa chama cha Muslim Brotherhood kitahodhi uchaguzi uliopangwa kufanywa mwezi Septemba, kwa sababu hakuna chama kisichokuwa cha kidini kilichoundwa kuchukua nafasi ya chama cha Bwana Mubarak, ambacho kimepigwa marufuku.
Mkutano unazungumza juu ya wagombea uchaguzi na mabadiliko zaidi ya katiba.
Lakini wanaharakati wengi hawana uzoefu, na wengine hawataki kuingia kwenye siasa.
Haijulikani vipi mkutano wa siku moja utaweza kuleta msimamo mmoja kati ya waakilishi wengi hivo.
Na uchaguzi unakaribia, hakuna muda wa kuunda chama kipya cha siasa.
No comments:
Post a Comment