Tuesday, 3 May 2011

Uefa yatupa lawama za Barca na Madrid

Shirikisho la Soka barani Ulaya-Uefa, limetupilia mbali malaalmiko yaliyowasilishwa na vilabu vya Real Madrid na Barcelona, kufuatia mchezo wao wa kwanza wa nusu fainali ya Ubingwa wa Ulaya.
Vurugu za wachezaji na maafisa wa Madridi na Barca
Vurugu za wachezaji na maafisa wa Madridi na Barca
Uefa imesema hakukuwa na "mikakati yoyote ya uchokozi" kwa Barca baada ya Real kudai Barcelona wanahatia ya "utovu wa nidhamu kinyume na michezo".
Uamuzi wa kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa mlinzi wa Real Madrid, Pepe unabakia pelepale, huku madai kumhusu meneja wa Real, Jose Mourinho yamekataliwa.
Lakini Uefa itachunguza madai yote yaliyowasilishwa dhidi ya vilabu hivyo viwili.
Taarifa ya Uefa imesema: "FC Barcelona imekwishawasilisha malalamiko yake dhidi ya Mourinho, yatakayosikilizwa na kamati ya udhibiti na nidhamu ya Uefa siku ya Ijumaa, tarehe 6 mwezi wa Mei.
"Hakuna hatua mpya za nidhamu zitakazochukuliwa dhidi ya Jose Mourinho kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Barcelona."
Barcelona wametuhumiwa kutokana na kadi nyekundu aliyooneshwa mlinda mlango wao wa akiba Jose Pinto wakati wa mapumziko.
Joto la mechi hiyo lilipandishwa zaidi na Mourinho baada ya filimbi ya mapumziko kupulizwa, alipodai Barcelona wanapendelewa na waamuzi.
Barcelona baada ya mkutano wa bodi uliofanyika siku ya Alhamisi iliyopita, wanaamini Mourinho kocha wa zamani wa vilabu vya Chelsea, Inter Milan na FC Porto "alivuka mipaka" kutokana na kauli yake.
Na Real ikajibu kwa kudai wachezaji wa Barca "kwa makusudi walikuwa wamemzonga mwamuzi kwa lengo la kumpotosha atoe uamuzi usiokubalika."
Uamuzi wa kukataa malalamiko yao ulichukuliwa na makamu mwenyekiti wa jopo la kamati ya nidhamu ya Uefa na uamuzi wa kukata rufaa upo wazi ndani ya siku tatu iwapo vilabu hivyo vitafikiria kufanya hivyo.

No comments: