Wednesday, 4 May 2011

OSAMA AMEJAA TELEE


Sifael Paul na Mashirika ya Kimataifa
Nyuma ya taarifa ya kifo cha kiongozi wa kundi la kigaidi duniani la Al-Qaeda, Osama bin Mohammed bin Awad bin Laden (54), kuna utata mtupu ikielezwa kwamba inawezekana jamaa huyo akawa hajafa, Risasi Mchanganyiko linashuka nayo hatua kwa hatua.

Taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia Jumatatu ya Mei 2, 2011 na kuthibitishwa na Rais wa Marekani, Barack Hussein Obama ilisema kuwa, Osama aliyezaliwa Machi 10, 1957 aliuawa na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo katika eneo la Abbottabad nchini Pakistan alikokuwa amejificha.

Kwa mujibu wa mtandao mmoja nchini Pakistan muda mfupi baada ya kutolewa taarifa hiyo, tukio hilo lilikosa ushahidi wa kutosha kuuthibitishia ulimwengu namna kiongozi huyo alivyouawa.

“Tunachojua Osama ni mzima. Haitoshi kusema ameuawa bila ushahidi wowote na isitoshe picha iliyotolewa ni ile ya Osama ya miaka kumi iliyopita.

“Ameuawa vipi? Ina maana sisi wote tunaamini kile wanachokisema Wamarekani bila uthibitisho? Hata kama ni hivyo, watu hawawezi kuamini kuwa alishakufa siku nyingi kwa ugonjwa?

“Tunachojua alikuwa mgonjwa tangu alipohusishwa na mashambulizi ya Septemba 11, 2001,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
JUMATATU SAA 12:50 ASUBUHI
Vichwa vya habari katika vyombo mbalimbali nchini India vilidai kwamba kama tukio hilo ni kweli, basi Pakistan itakuwa chaka la kuhifadhi magaidi.

SAA 12: 57 ASUBUHI
Taarifa ziliendelea kusambaa duniani kama moto wa kifuu ambapo Waziri Mkuu wa Australia, Julia Gillard alionya kuwa, kuuawa (kama ni kweli) kwa Osama siyo mwisho wa vita dhidi ya Kundi la Al-Qaeda hivyo akautaka ulimwengu kuongeza bidii ya kumaliza ugaidi.

SAA 1: 23 ASUBUHI
Picha yenye utata ya Osama ikimuonesha akiwa ameuwa iliendelea kusambaa mitandaoni duniani kote.

Kituo cha Runinga cha Pakistan kiliielezea picha hiyo ya ‘mzoga’ wa Osama kuwa ilikuwa ni ‘feki’.

SAA 1:58 ASUBUHI
Mtandao wa nchini Pakistan wa Jihadist Forums uliripoti kwa Lugha ya Kiarabu kuwa, Mungu aepushie mbali taarifa hiyo kwani Obama atakuwa amejiweka pabaya.

Ilisomeka: “Osama anaweza kuuawa lakini harakati zake hazitakufa kamwe.

“Kama kweli alikuwa ameuawa, taarifa ilipaswa kutolewa na Al-Qaeda na siyo Obama au Wamarekani.”

SAA 2:10 ASUBUHI
Shirika la Habari la Uingereza (BBC) liliripoti kuwa, Watalibani waligoma kusema chochote juu ya taarifa hiyo kwa kuwa hawakuiamini na uchunguzi ukawa unaendelea.

SAA 2: 45 ASUBUHI
Gazeti la nchini Marekani la The New York Times liliingia mtaani na ‘stori’ iliyokuwa ikieleza kwamba, mwili wa Osama ulipelekwa Afghanistan na kuzikwa baharini huku kukiwa hakuna ushahidi wowote, jambo lililoongeza utata wa tukio hilo.

SAA 3: 04 ASUBUHI
Mwandishi wa Gazeti la Telegraph la Uingereza, Ben Farmer, akiwa Kabul, Afghanistan alisema kuwa, muda mfupi kabla ya taarifa ya kuuawa kwa kiongozi huyo, magazeti nchini humo yaliripoti milipuko ya mabomu iliyokuwa ikisikika eneo la Abbottabad.

Alisema: “Milipuko mitatu ya mabomu ilisikika jirani na Kambi ya Jeshi la Pakistan na baadaye ndege za kijeshi zilionekana zikikatiza angani lakini hakukuwa na taarifa ya kuuawa kwa Osama.”

SAA 3: 25 ASUBUHI
Mwandishi Ben Farmer alizungumza na aliyewahi kuwa mkuu wa upelelezi wa Afghanistan, Amrullah Saleh ambaye alisema kuwa, Osama alikuwa amejificha Pakistan.

SAA 4: 07 ASUBUHI
Habari zilizosambazwa mitandaoni nchini Afghanistan zilisema kuwa, kwa mujibu wa watu wa karibu wa Kundi la Al- Qaeda: “Osama amejaa telee…” huku wakidai kwamba taarifa ya Obama ililenga kumchuria kifo.
MASWALI 10 TATA
1: Osama aliuawa vipi?

2: Kwa nini taarifa ya kifo cha Osama isitangazwe na Al-Qaeda wenyewe hadi itangazwe na Obama?

3: Kwa nini picha ya Osama ya miaka kumi itumike katika tukio hilo?

4: Kwa nini Wamarekani wasisambaze picha za tukio hilo kama walivyofanya kwa Saddam Hussein?

5: Kwa nini mwili wa Osama uzikwe haraka baharini?

6: Kwa nini ameuawa sasa hivi na siyo miaka 10 iliyopita kwani Wamarekani wanaaminika kuwa na mbinu nyingi?

7: Je, Osama hakufa siku nyingi kwa sababu alikuwa mgonjwa?

8: Kuuawa kwa Osama hakuna uhusiano wowote na uchaguzi wa Marekani mwaka ujao?

9: Je, tukio hilo (kama la kweli) lina madhara kiasi gani kwa raia wa Afghanistan?

10: Je, ndiyo mwisho wa dunia ukizingatia hali mbaya ya kisiasa katika nchini za Kiarabu?

Maswali haya tata yanafanya asilimia kubwa ya watu waliozungumza na Risasi Mchanganyiko kulifikiria tofauti tukio hilo.

No comments: